Kiswahili: Biblica® Open Kiswaili Contemporary Bible™

Updated ? hours ago # views See on DCS

Maombolezo

Chapter 1

    [1] 1 Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa,

         mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu!

     Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane,

         ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa!

     Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo

         sasa amekuwa mtumwa.

 

     2 Kwa uchungu, hulia sana usiku,

         machozi yapo kwenye mashavu yake.

     Miongoni mwa wapenzi wake wote

         hakuna yeyote wa kumfariji.

     Rafiki zake wote wamemsaliti,

         wamekuwa adui zake.

 

     3 Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili,

         Yuda amekwenda uhamishoni.

     Anakaa miongoni mwa mataifa,

         hapati mahali pa kupumzika.

     Wote ambao wanamsaka wamemkamata

         katikati ya dhiki yake.

 

     4 Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza,

         kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja

         kwenye sikukuu zake zilizoamriwa.

     Malango yake yote yamekuwa ukiwa,

         makuhani wake wanalia kwa uchungu,

     wanawali wake wanahuzunika,

         naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.

 

     5 Adui zake wamekuwa mabwana zake,

         watesi wake wana raha.

     Bwana amemletea huzuni

         kwa sababu ya dhambi zake nyingi.

     Watoto wake wamekwenda uhamishoni,

         mateka mbele ya adui.

 

     6 Fahari yote imeondoka

         kutoka kwa Binti Sayuni.

     Wakuu wake wako kama ayala

         ambaye hapati malisho,

     katika udhaifu wamekimbia

         mbele ya anayewasaka.

 

     7 Katika siku za mateso yake na kutangatanga,

         Yerusalemu hukumbuka hazina zote

         ambazo zilikuwa zake siku za kale.

     Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui,

         hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia.

     Watesi wake walimtazama

         na kumcheka katika maangamizi yake.

 

     8 Yerusalemu ametenda dhambi sana

         kwa hiyo amekuwa najisi.

     Wote waliomheshimu wanamdharau,

         kwa maana wameuona uchi wake.

     Yeye mwenyewe anapiga kite

         na kugeukia mbali.

 

     9 Uchafu wake umegandamana na nguo zake;

         hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye.

     Anguko lake lilikuwa la kushangaza,

         hapakuwepo na yeyote wa kumfariji.

     “Tazama, Ee Bwana , teso langu,

         kwa maana adui ameshinda.”

 

     10 Adui ametia mikono

         juu ya hazina zake zote,

     aliona mataifa ya kipagani

         wakiingia mahali patakatifu pake,

     wale uliowakataza kuingia

         kwenye kusanyiko lako.

 

     11 Watu wake wote wanalia kwa uchungu

         watafutapo chakula;

     wanabadilisha hazina zao kwa chakula

         ili waweze kuendelea kuishi.

     “Tazama, Ee Bwana , ufikiri,

         kwa maana nimedharauliwa.”

 

     12 “Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando?

         Angalieni kote mwone.

     Je, kuna maumivu kama maumivu yangu

         yale yaliyotiwa juu yangu,

     yale Bwana aliyoyaleta juu yangu

         katika siku ya hasira yake kali?

 

     13 “Kutoka juu alipeleka moto,

         akaushusha katika mifupa yangu.

     Aliitandia wavu miguu yangu

         na akanirudisha nyuma.

     Akanifanya mkiwa,

         na mdhaifu mchana kutwa.

 

     14 “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira,

         kwa mikono yake zilifumwa pamoja.

     Zimefika shingoni mwangu

         na Bwana ameziondoa nguvu zangu.

     Amenitia mikononi mwa wale

         ambao siwezi kushindana nao.

 

     15 “Bwana amewakataa wapiganaji wa vita

         wote walio kati yangu,

     ameagiza jeshi dhidi yangu

         kuwaponda vijana wangu wa kiume.

     Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga

         Bikira Binti Yuda.

 

     16 “Hii ndiyo sababu ninalia

         na macho yangu yanafurika machozi.

     Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji,

         hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu.

     Watoto wangu ni wakiwa

         kwa sababu adui ameshinda.”

 

     17 Sayuni ananyoosha mikono yake,

         lakini hakuna yeyote wa kumfariji.

     Bwana ametoa amri kwa ajili ya Yakobo

         kwamba majirani zake wawe adui zake;

         Yerusalemu umekuwa

         kitu najisi miongoni mwao.

 

     18 Bwana ni mwenye haki,

         hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake.

     Sikilizeni, enyi mataifa yote,

         tazameni maumivu yangu.

     Wavulana wangu na wasichana wangu

         wamekwenda uhamishoni.

 

     19 “Niliita washirika wangu

         lakini walinisaliti.

     Makuhani wangu na wazee wangu

         waliangamia mjini

     walipokuwa wakitafuta chakula

         ili waweze kuishi.

 

     20 “Angalia, Ee Bwana , jinsi nilivyo katika dhiki!

         Nina maumivu makali ndani yangu,

     nami ninahangaika moyoni mwangu,

         kwa kuwa nimekuwa mwasi sana.

     Huko nje, upanga unaua watu,

         ndani, kipo kifo tu.

 

     21 “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu,

         lakini hakuna yeyote wa kunifariji.

     Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu,

         wanafurahia lile ulilolitenda.

     Naomba uilete siku uliyoitangaza

         ili wawe kama mimi.

 

     22 “Uovu wao wote na uje mbele zako;

         uwashughulikie wao

     kama vile ulivyonishughulikia mimi

         kwa sababu ya dhambi zangu zote.

     Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi

         na moyo wangu umedhoofika.”


1: [1] Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

Chapter 2

    [1] 1 Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni

         kwa wingu la hasira yake!

     Ameitupa chini fahari ya Israeli

         kutoka mbinguni mpaka duniani,

     hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu

         katika siku ya hasira yake.

 

     2 Bila huruma Bwana ameyameza

         makao yote ya Yakobo;

     katika ghadhabu yake amebomoa

         ngome za Binti Yuda.

     Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake

         chini kwa aibu.

 

     3 Katika hasira kali amevunja

         kila pembe [2] ya Israeli.

     Ameuondoa mkono wake wa kuume

         alipokaribia adui.

     Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao

         ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.

 

     4 Ameupinda upinde wake kama adui,

         mkono wake wa kuume uko tayari.

     Kama vile adui amewachinja

         wote waliokuwa wanapendeza jicho,

     amemwaga ghadhabu yake kama moto

         juu ya hema la Binti Sayuni.

 

     5 Bwana ni kama adui;

         amemmeza Israeli.

     Amemeza majumba yake yote ya kifalme

         na kuangamiza ngome zake.

     Ameongeza huzuni na maombolezo

         kwa ajili ya Binti Yuda.

 

     6 Ameharibu maskani yake kama bustani,

         ameharibu mahali pake pa mkutano.

     Bwana amemfanya Sayuni kusahau

         sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;

     katika hasira yake kali amewadharau

         mfalme na kuhani.

 

     7 Bwana amekataa madhabahu yake

         na kuacha mahali patakatifu pake.

     Amemkabidhi adui kuta

         za majumba yake ya kifalme;

     wamepiga kelele katika nyumba ya Bwana

         kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.

 

     8 Bwana alikusudia kuangusha

         ukuta uliomzunguka Binti Sayuni.

     Ameinyoosha kamba ya kupimia

         na hakuuzuia mkono wake usiangamize.

     Alifanya maboma na kuta ziomboleze,

         vyote vikaharibika pamoja.

 

     9 Malango yake yamezama ardhini,

         makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.

     Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni

         miongoni mwa mataifa,

         sheria haipo tena,

     na manabii wake hawapati tena

         maono kutoka kwa Bwana .

 

     10 Wazee wa Binti Sayuni

         wanaketi chini kimya,

     wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao

         na kuvaa nguo za gunia.

     Wanawali wa Yerusalemu

         wamesujudu hadi ardhini.

 

     11 Macho yangu yamedhoofika kwa kulia,

         nina maumivu makali ndani,

     moyo wangu umemiminwa ardhini

         kwa sababu watu wangu wameangamizwa,

     kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia

         kwenye barabara za mji.

 

     12 Wanawaambia mama zao,

         “Wapi mkate na divai?”

     wazimiapo kama watu waliojeruhiwa

         katika barabara za mji,

     maisha yao yadhoofikavyo

         mikononi mwa mama zao.

 

     13 Ninaweza kusema nini kwa ajili yako?

         Nikulinganishe na nini,

         ee Binti Yerusalemu?

     Nitakufananisha na nini,

         ili nipate kukufariji,

         ee Bikira Binti Sayuni?

     Jeraha lako lina kina kama bahari.

         Ni nani awezaye kukuponya?

 

     14 Maono ya manabii wako

         yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu,

     hawakuifunua dhambi yako

         ili kukuzuilia kwenda utumwani.

     Maneno waliyokupa

         yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.

 

     15 Wote wapitiao njia yako

         wanakupigia makofi,

     wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao

         kwa Binti Yerusalemu:

     “Huu ndio ule mji ulioitwa

         mkamilifu wa uzuri,

         furaha ya dunia yote?”

 

     16 Adui zako wote wanapanua

         vinywa vyao dhidi yako,

     wanadhihaki na kusaga meno yao

         na kusema, “Tumemmeza.

     Hii ndiyo siku tuliyoingojea,

         tumeishi na kuiona.”

 

     17 Bwana amefanya lile alilolipanga;

         ametimiza neno lake

         aliloliamuru siku za kale.

     Amekuangusha bila huruma,

         amewaacha adui wakusimange,

         ametukuza pembe ya adui yako.

 

     18 Mioyo ya watu

         inamlilia Bwana.

     Ee ukuta wa Binti Sayuni,

         machozi yako na yatiririke kama mto

         usiku na mchana;

     usijipe nafuu,

         macho yako yasipumzike.

 

     19 Inuka, lia usiku,

         zamu za usiku zianzapo;

     mimina moyo wako kama maji

         mbele za Bwana.

     Mwinulie yeye mikono yako

         kwa ajili ya maisha ya watoto wako,

     ambao wanazimia kwa njaa

         kwenye kila mwanzo wa barabara.

 

     20 “Tazama, Ee Bwana , ufikirie:

         Ni nani ambaye umepata

         kumtendea namna hii?

     Je, wanawake wakule wazao wao,

         watoto waliowalea?

     Je, kuhani na nabii auawe

         mahali patakatifu pa Bwana?

 

     21 “Vijana na wazee hujilaza pamoja

         katika mavumbi ya barabarani,

     wavulana wangu na wasichana

         wameanguka kwa upanga.

     Umewaua katika siku ya hasira yako,

         umewachinja bila huruma.

 

     22 “Kama ulivyoita siku ya karamu,

         ndivyo ulivyoagiza hofu kuu

         dhidi yangu kila upande.

     Katika siku ya hasira ya Bwana

         hakuna yeyote aliyekwepa au kupona;

     wale niliowatunza na kuwalea,

         adui yangu amewaangamiza.”


2:3 [2] Pembe inawakilisha nguvu; pia 2:17.
2:22 [1] Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

Chapter 3

    [1] 1 Mimi ndiye mtu aliyeona mateso

         kwa fimbo ya ghadhabu yake.

     2 Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee

         gizani wala si katika nuru;

     3 hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu

         tena na tena, mchana kutwa.

 

     4 Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa

         na ameivunja mifupa yangu.

     5 Amenizingira na kunizunguka

         kwa uchungu na taabu.

     6 Amenifanya niishi gizani

         kama wale waliokufa.

 

     7 Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka,

         amenifunga kwa minyororo mizito.

     8 Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada,

         anakataa kupokea maombi yangu.

     9 Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe,

         amepotosha njia zangu.

 

     10 Kama dubu aviziaye,

         kama simba mafichoni,

     11 ameniburuta kutoka njia,

         akanirarua na kuniacha bila msaada.

     12 Amevuta upinde wake

         na kunifanya mimi niwe lengo

         kwa ajili ya mishale yake.

 

     13 Alinichoma moyo wangu kwa mishale

         iliyotoka kwenye podo lake.

     14 Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote,

         wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.

     15 Amenijaza kwa majani machungu

         na kunishibisha kwa nyongo.

 

     16 Amevunja meno yangu kwa changarawe,

         amenikanyagia mavumbini.

     17 Amani yangu imeondolewa,

         nimesahau kufanikiwa ni nini.

     18 Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka

         na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Bwana .”

 

     19 Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu,

         uchungu na nyongo.

     20 Ninayakumbuka vyema,

         nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.

     21 Hata hivyo najikumbusha neno hili

         na kwa hiyo ninalo tumaini.

 

     22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana , hatuangamii,

         kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

     23 Ni mpya kila asubuhi,

         uaminifu wako ni mkuu.

     24 Nimeiambia nafsi yangu, “ Bwana ni fungu langu,

         kwa hiyo nitamngojea.”

 

     25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

         kwa yule ambaye humtafuta;

     26 ni vyema kungojea kwa utulivu

         kwa ajili ya wokovu wa Bwana .

     27 Ni vyema mtu kuchukua nira

         bado angali kijana.

 

     28 Na akae peke yake awe kimya,

         kwa maana Bwana ameiweka juu yake.

     29 Na azike uso wake mavumbini

         bado panawezekana kuwa na matumaini.

     30 Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye,

         na ajazwe na aibu.

 

     31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali

         na Bwana milele.

     32 Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma,

         kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.

     33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso

         au huzuni watoto wa wanadamu.

 

     34 Kuwaponda chini ya nyayo

         wafungwa wote katika nchi,

     35 Kumnyima mtu haki zake

         mbele za Aliye Juu Sana,

     36 kumnyima mtu haki:

         Je, Bwana asione mambo kama haya?

 

     37 Nani awezaye kusema nalo likatendeka

         kama Bwana hajaamuru?

     38 Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana

         ndiko yatokako maafa na mambo mema?

     39 Mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika

         wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?

 

     40 Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu,

         na tumrudie Bwana Mungu.

     41 Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu

         kwa Mungu mbinguni, na tuseme:

     42 “Tumetenda dhambi na kuasi

         nawe hujasamehe.

 

     43 “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia;

         umetuchinja bila huruma.

     44 Unajifunika mwenyewe kwa wingu,

         ili pasiwe na ombi

         litakaloweza kupenya.

     45 Umetufanya takataka na uchafu

         miongoni mwa mataifa.

 

     46 “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao

         wazi dhidi yetu.

     47 Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula,

         uharibifu na maangamizi.”

     48 Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu,

         kwa sababu watu wangu wameangamizwa.

 

     49 Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma,

         bila kupata nafuu,

     50 hadi Bwana atazame chini

         kutoka mbinguni na kuona.

     51 Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini

         kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.

 

     52 Wale waliokuwa adui zangu bila sababu

         wameniwinda kama ndege.

     53 Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo

         na kunitupia mawe;

     54 maji yalifunika juu ya kichwa changu,

         nami nikafikiri nilikuwa karibu

         kukatiliwa mbali.

 

     55 Nililiitia jina lako, Ee Bwana ,

         kutoka vina vya shimo.

     56 Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako

         kilio changu nikuombapo msaada.”

     57 Ulikuja karibu nilipokuita,

         nawe ukasema, “Usiogope.”

 

     58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu,

         ukaukomboa uhai wangu.

     59 Umeona, Ee Bwana , ubaya niliotendewa.

         Tetea shauri langu!

     60 Umeona kina cha kisasi chao,

         mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.

 

     61 Ee Bwana , umesikia matukano yao,

         mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:

     62 kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia

         dhidi yangu mchana kutwa.

     63 Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama,

         wananidhihaki katika nyimbo zao.

 

     64 Uwalipe kile wanachostahili, Ee Bwana ,

         kwa yale ambayo mikono yao imetenda.

     65 Weka pazia juu ya mioyo yao,

         laana yako na iwe juu yao!

     66 Wafuatilie katika hasira na uwaangamize

         kutoka chini ya mbingu za Bwana .


3:22 [1] Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

Chapter 4

    [1] 1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake,

         dhahabu iliyo safi haingʼai!

     Vito vya thamani vimetawanywa

         kwenye mwanzo wa kila barabara.

 

     2 Wana wa Sayuni wenye thamani,

         ambao mwanzo uzito wa thamani yao

         ulikuwa wa dhahabu,

     sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,

         kazi ya mikono ya mfinyanzi!

 

     3 Hata mbweha hutoa matiti yao

         kunyonyesha watoto wao,

     lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma

         kama mbuni jangwani.

 

     4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga

         umegandamana na kaakaa la kinywa chake,

     watoto huomba mkate,

         lakini hakuna yeyote awapaye.

 

     5 Wale waliokula vyakula vya kifahari

         ni maskini barabarani.

     Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau

         sasa wanalalia majivu.

 

     6 Adhabu ya watu wangu

         ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,

     ambayo ilipinduliwa ghafula

         bila kuwepo mkono wa msaada.

 

     7 Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji

         na weupe kuliko maziwa,

     miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,

         kuonekana kwao kama yakuti samawi.

 

     8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;

         hawatambulikani barabarani.

     Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,

         imekuwa mikavu kama fimbo.

 

     9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora

         kuliko wale wanaokufa njaa;

     wanateseka kwa njaa, wanatokomea

         kwa kukosa chakula kutoka shambani.

 

     10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma

         wanapika watoto wao wenyewe,

     waliokuwa chakula chao

         watu wangu walipoangamizwa.

 

     11 Bwana ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;

         ameimwaga hasira yake kali.

     Amewasha moto katika Sayuni

         ambao umeteketeza misingi yake.

 

     12 Wafalme wa dunia hawakuamini,

         wala mtu yeyote wa duniani,

     kwamba adui na watesi wangeweza kuingia

         kwenye malango ya Yerusalemu.

 

     13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,

         na maovu ya makuhani wake,

     waliomwaga ndani yake

         damu ya wenye haki.

 

     14 Sasa wanapapasa papasa barabarani

         kama watu ambao ni vipofu.

     Wamenajisiwa kabisa kwa damu,

         hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.

 

     15 Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!

         Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”

     Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko,

         watu miongoni mwa mataifa wanasema,

         “Hawawezi kukaa hapa zaidi.”

 

     16 Bwana mwenyewe amewatawanya;

         hawaangalii tena.

     Makuhani hawaonyeshwi heshima,

         wazee hawakubaliki.

 

     17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,

         kwa kutazamia bure msaada;

     tuliangalia kutoka minara yetu

         kwa taifa lisiloweza kutuokoa.

 

     18 Watu walituvizia katika kila hatua

         hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.

     Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,

         kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.

 

     19 Waliotufuatia walikuwa wepesi

         kuliko tai angani;

         walitusaka juu milimani

         na kutuvizia jangwani.

 

     20 Mpakwa mafuta wa Bwana , pumzi ya uhai wetu hasa,

         alinaswa katika mitego yao.

     Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake

         tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.

 

     21 Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,

         wewe unayeishi nchi ya Usi.

     Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,

         Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.

 

     22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,

         hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.

     Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako,

         na atafunua uovu wako.


4:66 [1] Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

Chapter 5

     1 Kumbuka, Ee Bwana , yaliyotupata,

         tazama, nawe uione aibu yetu.

     2 Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,

         na nyumba zetu kwa wageni.

     3 Tumekuwa yatima wasio na baba,

         mama zetu wamekuwa kama wajane.

     4 Ni lazima tununue maji tunayokunywa,

         kuni zetu zapatikana tu kwa kununua.

     5 Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,

         tumechoka na hakuna pumziko.

     6 Tumejitolea kwa Misri na Ashuru

         tupate chakula cha kutosha.

     7 Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,

         na sisi tunachukua adhabu yao.

     8 Watumwa wanatutawala

         na hakuna wa kutuokoa mikononi yao.

     9 Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu

         kwa sababu ya upanga jangwani.

     10 Ngozi yetu ina joto kama tanuru,

         kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa.

     11 Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,

         na mabikira katika miji ya Yuda.

     12 Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,

         wazee hawapewi heshima.

     13 Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia,

         wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.

     14 Wazee wameondoka langoni la mji,

         vijana wameacha kuimba nyimbo zao.

     15 Furaha imeondoka mioyoni mwetu,

         kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.

     16 Taji imeanguka kutoka kichwani petu.

         Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi!

     17 Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia,

         kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia,

     18 kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa,

         nao mbweha wanatembea juu yake.

     19 Wewe, Ee Bwana unatawala milele,

         kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi.

     20 Kwa nini watusahau siku zote?

         Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?

     21 Turudishe kwako mwenyewe, Ee Bwana ,

         ili tupate kurudi.

         Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,

     22 isipokuwa uwe umetukataa kabisa

         na umetukasirikia pasipo kipimo.