Kiswahili: Biblica® Open Kiswaili Contemporary Bible™

Updated ? hours ago # views See on DCS

Hosea

Chapter 1

1 Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli.

 

Mke Wa Hosea Na Watoto

2 Wakati Bwana alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, Bwana alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha Bwana .” 3 Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana.

4 Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Yezreeli, [1] kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli. 5 Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”

6 Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, [2] kwa maana sitaonyesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe. 7 Hata hivyo nitaonyesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kwa njia ya Bwana Mungu wao.”

8 Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine. 9 Kisha Bwana akasema, “Mwite Lo-Ami [3] kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu.

10 “Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ 11 Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.


1:4 [1] Yezreeli maana yake Mungu hupanda.
1:6 [2] Lo-Ruhama maana yake Sio mpenzi wangu.
1:9 [3] Lo-Ami maana yake Sio watu wangu.

Chapter 2

1 “Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’

Israeli Aadhibiwa Na Kurudishwa

     2 “Mkemeeni mama yenu, mkemeeni,

         kwa maana yeye si mke wangu,

         nami si mume wake.

     Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake

         na uzinzi kati ya matiti yake.

     3 Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi

         na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa.

     Nitamfanya kama jangwa,

         nitamgeuza awe nchi ya kiu,

         nami nitamuua kwa kiu.

     4 Sitaonyesha upendo wangu kwa watoto wake,

         kwa sababu ni watoto wa uzinzi.

     5 Mama yao amekosa uaminifu

         na amewachukua mimba katika aibu.

     Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,

         ambao hunipa chakula changu

         na maji yangu,

     sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu

         na kinywaji changu.’

     6 Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake

         kwa vichaka vya miiba,

     nitamjengea ukuta ili kwamba

         asiweze kutoka.

     7 Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata;

         atawatafuta lakini hatawapata.

     Kisha atasema,

         ‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza,

     kwa maana nilikuwa na hali njema zaidi

         kuliko sasa.’

     8 Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye

         niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta,

     niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia

         kwa kumtumikia Baali.

 

     9 “Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa

         na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari.

     Nitamnyangʼanya sufu yangu na kitani yangu

         iliyokusudiwa kufunika uchi wake.

     10 Basi sasa nitaufunua ufisadi wake

         mbele ya wapenzi wake;

     hakuna yeyote atakayemtoa

         mikononi mwangu.

     11 Nitakomesha furaha na macheko yake yote:

         sikukuu zake za mwaka,

         sikukuu za Miandamo ya Mwezi,

         siku zake za Sabato,

         sikukuu zake zote zilizoamriwa.

     12 Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake,

         ambayo alisema yalikuwa malipo yake

         kutoka kwa wapenzi wake;

     nitaifanya kuwa kichaka,

         nao wanyama pori wataila.

     13 Nitamwadhibu kwa ajili ya siku

         alizowafukizia uvumba Mabaali;

     alipojipamba kwa pete

         na kwa vito vya thamani,

     na kuwaendea wapenzi wake,

         lakini mimi alinisahau,” asema Bwana .

 

     14 “Kwa hiyo sasa nitamshawishi;

         nitamwongoza hadi jangwani

         na kuzungumza naye kwa upole.

     15 Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,

         nami nitalifanya Bonde la Akori [1]

         mlango wa matumaini.

     Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake,

         kama siku zile alizotoka Misri.

 

     16 “Katika siku ile,” asema Bwana ,

         “utaniita mimi ‘Mume wangu’;

         hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’

     17 Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka midomoni mwake,

         wala hataomba tena kwa majina yao.

     18 Katika siku ile nitafanya Agano kwa ajili yao

         na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani,

         na viumbe vile vitambaavyo ardhini.

     Upinde, upanga na vita,

         nitaondolea mbali katika nchi,

         ili kwamba wote waweze kukaa salama.

     19 Nitakuposa uwe wangu milele;

         nitakuposa kwa uadilifu na haki,

         kwa upendo na huruma.

     20 Nitakuposa kwa uaminifu,

         nawe utamkubali Bwana .

 

     21 “Katika siku ile nitajibu,”

         asema Bwana ,

     “nitajibu kwa anga,

         nazo anga zitajibu kwa nchi;

     22 nayo nchi itajibu kwa nafaka,

         divai mpya na mafuta,

         navyo vitajibu kwa Yezreeli.

     23 Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;

         nami nitaonyesha pendo langu kwake

         yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu. [2]

     Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu,’ [3]

         ‘Ninyi ni watu wangu’;

         nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”


2:15 [1] Akori maana yake ni Taabu.
2:23 [2] Kiebrania ni Lo-Ruhama.
2:23 [3] Kiebrania ni Lo-Ami.

Chapter 3

Upatanisho Wa Hosea Na Mkewe

1 Bwana akaniambia, “Nenda, ukaonyeshe upendo wako kwa mke wako tena, ingawa amependwa na mwingine naye ni mzinzi. Mpende kama Bwana apendavyo Waisraeli, ingawa wanageukia miungu mingine na kupenda mikate mitamu ya zabibu kavu iliyowekwa wakfu.”

2 Basi nilimnunua huyo mwanamke kwa shekeli kumi na tano [1] za fedha, pia kwa kiasi kama cha homeri moja na nusu [2] ya shayiri. 3 Kisha nilimwambia, “Utaishi nami kwa siku nyingi, hupaswi kuwa kahaba au kuwa na uhusiano wa karibu na mtu yeyote, nami nitaishi na wewe.”

4 Kwa maana Waisraeli wataishi siku nyingi bila kuwa na mfalme wala mkuu, bila kuwa na dhabihu wala mawe matakatifu, bila kisibau wala sanamu. 5 Baadaye Waisraeli watarudi na kumtafuta Bwana Mungu wao na Daudi mfalme wao. Watakuja wakitetemeka kwa Bwana na kwa baraka zake katika siku za mwisho.


3:2 [1] Shekeli 15 za fedha ni sawa na gramu 170.
3:2 [2] Homeri moja na nusu ni kama lita 330.

Chapter 4

Shtaka Dhidi Ya Israeli

     1 Sikieni neno la Bwana , enyi Waisraeli,

         kwa sababu Bwana analo shtaka

         dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:

     “Hakuna uaminifu, hakuna upendo,

         hakuna kumjua Mungu katika nchi.

     2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,

         wizi na uzinzi,

     bila kuwa na mipaka,

         nao umwagaji damu mmoja

         baada ya mwingine.

     3 Kwa sababu hii nchi huomboleza,

         wote waishio ndani mwake wanadhoofika,

     wanyama wa kondeni, ndege wa angani

         na samaki wa baharini wanakufa.

 

     4 “Lakini mtu awaye yote na asilete shtaka,

         mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,

     kwa maana watu wako ni kama wale

         waletao mashtaka dhidi ya kuhani.

     5 Unajikwaa usiku na mchana,

         nao manabii hujikwaa pamoja nawe.

     Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:

         6 watu wangu wanaangamizwa

         kwa kukosa maarifa,

 

     “Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,

         mimi nami nitakukataa wewe

         usiwe kuhani kwangu mimi;

     kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako

         mimi nami sitawajali watoto wako.

     7 Kadiri makuhani walivyoongezeka,

         ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,

         walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.

     8 Hujilisha dhambi za watu wangu

         na kupendezwa na uovu wao.

     9 Hata itakuwa: Kama walivyo watu,

         ndivyo walivyo makuhani.

     Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao

         na kuwalipa kwa matendo yao.

 

     10 “Watakula lakini hawatashiba;

         watajiingiza katika ukahaba

         lakini hawataongezeka,

     kwa sababu wamemwacha Bwana

         na kujiingiza wenyewe

         11 katika ukahaba,

     divai ya zamani na divai mpya,

         ambavyo huondoa ufahamu

         12 wa watu wangu.

     Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti

         nao hujibiwa na fimbo ya mti.

     Roho ya ukahaba imewapotosha,

         hawana uaminifu kwa Mungu wao.

     13 Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima

         na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,

     chini ya mialoni, milibua na miela,

         ambako kuna vivuli vizuri.

     Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba

         na wake za wana wenu uzinzi.

 

     14 “Sitawaadhibu binti zenu wakati

         wanapogeukia ukahaba,

     wala wake za wana wenu

         wanapofanya uzinzi,

     kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya

         na kutambikia pamoja na makahaba

         wa mahali pa kuabudia miungu:

     watu wasiokuwa na ufahamu

         wataangamia!

 

     15 “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,

         Yuda naye asije akawa na hatia.

 

     “Usiende Gilgali,

         usipande kwenda Beth-Aveni [1]

     Wala usiape,

         ‘Hakika kama Bwana aishivyo!’

     16 Waisraeli ni wakaidi,

         kama mtamba wa ngʼombe ambaye ni mkaidi.

     Ni jinsi gani basi Bwana anaweza kuwachunga

         kama wana-kondoo

         katika shamba la majani?

     17 Efraimu amejiunga na sanamu,

         ondokana naye!

     18 Hata wakati wamemaliza vileo vyao

         wanaendelea na ukahaba wao,

     watawala wao hupenda sana

         njia za aibu.

     19 Kisulisuli kitawafagilia mbali

         na dhabihu zao zitawaletea aibu.


4:15 [1] Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka.

Chapter 5

Hukumu Dhidi Ya Israeli

     1 “Sikieni hili, enyi makuhani!

         Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli!

     Sikieni, ee nyumba ya mfalme!

         Hukumu hii ni dhidi yenu:

     Mmekuwa mtego huko Mispa,

         wavu uliotandwa juu ya Tabori.

     2 Waasi wamezidisha sana mauaji.

         Mimi nitawatiisha wote.

     3 Ninajua yote kuhusu Efraimu,

         Israeli hukufichika kwangu.

     Efraimu, sasa umegeukia ukahaba,

         Israeli amenajisika.

 

     4 “Matendo yao hayawaachii

         kurudi kwa Mungu wao.

     Roho ya ukahaba imo ndani ya mioyo yao,

         hawamkubali Bwana .

     5 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao;

         Waisraeli, hata Efraimu,

     wanajikwaa katika dhambi zao;

         pia Yuda atajikwaa pamoja nao.

     6 Wakati wanapokwenda na makundi yao

         ya kondoo na ngʼombe

         kumtafuta Bwana ,

     hawatampata;

         yeye amejiondoa kutoka kwao.

     7 Wao si waaminifu kwa Bwana ;

         wamezaa watoto haramu.

     Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi

         zitawaangamiza wao

         pamoja na mashamba yao.

 

     8 “Pigeni tarumbeta huko Gibea,

         baragumu huko Rama.

     Paza kilio cha vita huko Beth-Aveni, [1]

         ongoza, ee Benyamini.

     9 Efraimu ataachwa ukiwa

         katika siku ya kuadhibiwa.

     Miongoni mwa makabila ya Israeli

         ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.

     10 Viongozi wa Yuda ni kama wale

         wanaosogeza mawe ya mpaka.

     Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao

         kama mafuriko ya maji.

     11 Efraimu ameonewa,

         amekanyagwa katika hukumu

         kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.

     12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu,

         na kama uozo kwa watu wa Yuda.

 

     13 “Wakati Efraimu alipoona ugonjwa wake,

         naye Yuda vidonda vyake,

     ndipo Efraimu alipogeukia Ashuru,

         na kuomba msaada kwa mfalme mkuu.

     Lakini hawezi kukuponya,

         wala hawezi kukuponya vidonda vyako.

     14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu,

         kama simba mkubwa kwa Yuda.

     Nitawararua vipande vipande na kuondoka;

         nitawachukua mbali,

         na hakuna wa kuwaokoa.

     15 Kisha nitarudi mahali pangu

         mpaka watakapokubali kosa lao.

     Nao watautafuta uso wangu;

         katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”


5:8 [1] Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka.

Chapter 6

Israeli Asiye Na Toba

     1 “Njooni, tumrudie Bwana .

     Ameturarua vipande vipande

         lakini atatuponya;

     ametujeruhi lakini

         atatufunga majeraha yetu.

     2 Baada ya siku mbili atatufufua;

         katika siku ya tatu atatuinua,

         ili tuweze kuishi mbele zake.

     3 Tumkubali Bwana ,

         tukaze kumkubali yeye.

     Kutokea kwake ni hakika kama vile

         kuchomoza kwa jua;

     atatujia kama mvua za masika,

         kama vile mvua za vuli

         ziinyweshavyo nchi.”

 

     4 “Nifanye nini nawe, Efraimu?

         Nifanye nini nawe, Yuda?

     Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi,

         kama umande wa alfajiri utowekao.

     5 Kwa hiyo ninawakata ninyi vipande vipande

         kwa kutumia manabii wangu;

     nimewaua ninyi kwa maneno ya kinywa changu,

         hukumu zangu zinawaka

         kama umeme juu yenu.

     6 Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu,

         kumkubali Mungu zaidi

         kuliko sadaka za kuteketezwa.

     7 Wamevunja Agano kama Adamu:

         huko hawakuwa waaminifu kwangu.

     8 Gileadi ni mji wenye watu waovu,

         umetiwa madoa kwa nyayo za damu.

     9 Kama wanyangʼanyi wamviziavyo mtu,

         ndivyo magenge ya makuhani wafanyavyo;

     wanaulia watu kwenye njia iendayo Shekemu,

         wakifanya uhalifu wa aibu.

     10 Nimeona jambo la kutisha

         katika nyumba ya Israeli.

     Huko Efraimu amejitolea kwa ukahaba

         na Israeli amenajisika.

 

     11 “Pia kwa ajili yako, Yuda,

         mavuno yameamriwa.

 

     “Wakati wowote ningerejesha neema ya watu wangu,

Chapter 7

     1 kila mara nilipotaka kumponya Israeli,

         dhambi za Efraimu zinafichuliwa

         na maovu ya Samaria yanafunuliwa.

     Wanafanya udanganyifu,

         wevi huvunja nyumba,

         maharamia hunyangʼanya barabarani,

     2 lakini hawafahamu kwamba

         ninakumbuka matendo yao yote mabaya.

     Dhambi zao zimewameza,

         ziko mbele zangu siku zote.

 

     3 “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao,

         wakuu wao kwa uongo wao.

     4 Wote ni wazinzi,

         wanawaka kama tanuru

     ambayo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea

         kuanzia kukanda unga

         hadi umekwisha kuumuka.

     5 Katika sikukuu ya mfalme wetu

         wakuu wanawaka kwa mvinyo,

         naye anawaunga mkono wenye mizaha.

     6 Mioyo yao ni kama tanuru,

         wanamwendea kwa hila.

     Hasira yao inafoka moshi usiku kucha,

         wakati wa asubuhi inalipuka

         kama miali ya moto.

     7 Wote ni moto kama tanuru;

         wanawaangamiza watawala wao.

     Wafalme wake wote wanaanguka,

         wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.

 

     8 “Efraimu anajichanganya na mataifa;

         Efraimu ni mkate ambao haukuiva.

     9 Wageni wananyonya nguvu zake,

         lakini hafahamu hilo.

     Nywele zake zina mvi hapa na pale,

         lakini hana habari.

     10 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake,

         lakini pamoja na haya yote

     harudi kwa Bwana Mungu wake

         wala kumtafuta.

 

     11 “Efraimu ni kama hua,

         hudanganywa kwa urahisi na hana akili:

     mara anaita Misri,

         mara anageukia Ashuru.

     12 Wakati watakapokwenda,

         nitatupa wavu wangu juu yao;

     nitawavuta chini waanguke

         kama ndege wa angani.

     Nitakaposikia wakikusanyika pamoja,

         nitawanasa.

     13 Ole wao, kwa sababu

         wamepotoka kutoka kwangu!

     Maangamizi ni yao

         kwa sababu wameniasi!

     Ninatamani kuwakomboa,

         lakini wanasema uongo dhidi yangu.

     14 Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao,

         bali wanaomboleza vitandani mwao.

     Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya,

         lakini hugeukia mbali nami.

     15 Niliwafundisha na kuwatia nguvu,

         lakini wanapanga mabaya dhidi yangu.

     16 Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana,

         wako kama upinde wenye kasoro.

     Viongozi wao wataanguka kwa upanga

         kwa sababu ya maneno yao ya jeuri.

     Kwa ajili ya hili watadhihakiwa

         katika nchi ya Misri.

Chapter 8

Israeli Kuvuna Kisulisuli

     1 “Wekeni tarumbeta midomoni mwenu!

         Tai yuko juu ya nyumba ya Bwana

     kwa sababu watu wamevunja Agano langu,

         wameasi dhidi ya sheria yangu.

     2 Israeli ananililia,

         ‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’

     3 Lakini Israeli amekataa lile lililo jema,

         adui atamfuatia.

     4 Wanaweka wafalme bila idhini yangu,

         wamechagua wakuu bila kibali changu.

     Kwa fedha zao na dhahabu

         wamejitengenezea sanamu kwa ajili

         ya maangamizi yao wenyewe.

     5 Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama!

         Hasira yangu inawaka dhidi yao.

     Watakuwa najisi mpaka lini?

         6 Zimetoka katika Israeli!

     Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu.

         Atavunjwa vipande vipande,

         yule ndama wa Samaria.

 

     7 “Wanapanda upepo

         na kuvuna upepo wa kisulisuli.

     Bua halina suke,

         halitatoa unga.

     Kama lingetoa nafaka,

         wageni wangeila yote.

     8 Israeli amemezwa;

         sasa yupo miongoni mwa mataifa

         kama kitu kisicho na thamani.

     9 Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru

         kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake.

     Efraimu amejiuza mwenyewe

         kwa wapenzi.

     10 Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa,

         sasa nitawakusanya pamoja.

     Wataanza kudhoofika chini ya uonevu

         wa mfalme mwenye nguvu.

 

     11 “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi

         kwa ajili ya sadaka za dhambi,

     hizi zimekuwa madhabahu

         za kufanyia dhambi.

     12 Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi

         kuhusu sheria yangu,

     lakini wameziangalia

         kama kitu cha kigeni.

     13 Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi

         nao wanakula hiyo nyama,

         lakini Bwana hapendezwi nao.

     Sasa ataukumbuka uovu wao

         na kuadhibu dhambi zao:

         Watarudi Misri.

     14 Israeli amemsahau Muumba wake

         na kujenga majumba ya kifalme,

         Yuda amejengea miji mingi ngome.

     Lakini nitatuma moto kwenye miji yao

         utakaoteketeza ngome zao.”

Chapter 9

Adhabu Kwa Israeli

     1 Usifurahie, ee Israeli;

         usishangilie kama mataifa mengine.

     Kwa kuwa hukuwa

         mwaminifu kwa Mungu wako;

     umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu

         ya kupuria nafaka.

     2 Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai

         havitalisha watu,

         divai mpya itawapungukia.

     3 Hawataishi katika nchi ya Bwana ,

         Efraimu atarudi Misri

     na atakula chakula

         kilicho najisi huko Ashuru.

     4 Hawatammiminia Bwana sadaka ya divai

         wala dhabihu zao hazitampendeza.

     Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao

         kama mkate wa waombolezaji;

         nao wote wazilao watakuwa najisi.

     Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe;

         kisije katika Hekalu la Bwana .

 

     5 Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa,

         katika siku za sikukuu za Bwana ?

     6 Hata ikiwa wataokoka maangamizi,

         Misri atawakusanya,

         nayo Memfisi [1] itawazika.

     Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma,

         nayo miiba itafunika mahema yao.

     7 Siku za adhabu zinakuja,

         siku za malipo zimewadia.

         Israeli na afahamu hili.

     Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana

         na uadui wenu ni mkubwa sana,

     nabii anadhaniwa ni mpumbavu,

         mtu aliyeongozwa na Mungu

         anaonekana mwendawazimu.

     8 Nabii, pamoja na Mungu wangu,

         ndiye mlinzi juu ya Efraimu,

     hata hivyo mitego inamngojea

         katika mapito yake yote,

         na uadui katika nyumba ya Mungu wake.

     9 Wamezama sana katika rushwa,

         kama katika siku za Gibea.

     Mungu atakumbuka uovu wao

         na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.

 

     10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama

         kupata zabibu jangwani;

     nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona

         matunda ya kwanza katika mtini.

     Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu

         kwa ile sanamu ya aibu,

     nao wakawa najisi

         kama kitu kile walichokipenda.

     11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege:

         hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba,

         hakuna kutunga mimba.

     12 Hata wakilea watoto,

         nitamuua kila mmoja.

     Ole wao

         nitakapowapiga kisogo!

     13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro,

         aliyeoteshwa mahali pazuri.

     Lakini Efraimu wataleta

         watoto wao kwa mchinjaji.”

 

     14 Wape, Ee Bwana ,

         je, utawapa nini?

     Wape matumbo ya kuharibu mimba

         na matiti yaliyokauka.

 

     15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,

         niliwachukia huko.

     Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,

         nitawafukuza katika nyumba yangu.

     Sitawapenda tena,

         viongozi wao wote ni waasi.

     16 Efraimu ameharibiwa,

         mzizi wao umenyauka,

         hawazai tunda.

     Hata kama watazaa watoto,

         nitawachinja watoto wao

         waliotunzwa vizuri.”

 

     17 Mungu wangu atawakataa

         kwa sababu hawakumtii;

     watakuwa watu wa kutangatanga

         miongoni mwa mataifa.


9:6 [1] Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu.

Chapter 10

     1 Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,

         alijizalia matunda mwenyewe.

     Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,

         alijenga madhabahu zaidi;

     kadiri nchi yake ilivyostawi,

         alipamba mawe yake ya ibada.

     2 Moyo wao ni mdanganyifu,

         nao sasa lazima wachukue hatia yao.

     Bwana atabomoa madhabahu zao

         na kuharibu mawe yao ya ibada.

 

     3 Kisha watasema, “Hatuna mfalme

         kwa sababu hatukumheshimu Bwana .

     Lakini hata kama tungelikuwa na mfalme,

         angeweza kutufanyia nini?”

     4 Wanaweka ahadi nyingi,

         huapa viapo vya uongo

         wanapofanya mapatano;

     kwa hiyo mashtaka huchipuka

         kama magugu ya sumu

         katika shamba lililolimwa.

     5 Watu wanaoishi Samaria huogopa

         kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni. [1]

     Watu wake wataiombolezea,

         vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu,

     wale waliokuwa wamefurahia fahari yake,

         kwa sababu itaondolewa kutoka kwao

         kwenda uhamishoni.

     6 Itachukuliwa kwenda Ashuru

         kama ushuru kwa mfalme mkuu.

     Efraimu atafedheheshwa;

         Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.

     7 Samaria na mfalme wake wataelea

         kama kijiti juu ya uso wa maji.

     8 Mahali pa kuabudia sanamu pa uovu [2] pataharibiwa:

         ndiyo dhambi ya Israeli.

     Miiba na mibaruti itaota

         na kufunika madhabahu zao.

     Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!”

         na vilima, “Tuangukieni!”

 

     9 “Tangu siku za Gibea, mmetenda dhambi, ee Israeli,

         huko ndiko mlikobaki.

     Je, vita havikuwapata

         watenda mabaya huko Gibea?

     10 Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu;

         mataifa yatakusanywa dhidi yao

     ili kuwaweka katika vifungo

         kwa ajili ya dhambi zao mbili.

     11 Efraimu ni mtamba wa ngʼombe aliyefundishwa

         ambaye hupenda kupura,

     hivyo nitamfunga nira

         juu ya shingo yake nzuri.

     Nitamwendesha Efraimu,

         Yuda lazima alime,

     naye Yakobo lazima avunjavunje

         mabonge ya udongo.

     12 Jipandieni wenyewe haki,

         vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,

     vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;

         kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Bwana ,

     mpaka atakapokuja

         na kuwanyeshea juu yenu haki.

     13 Lakini mmepanda uovu,

         mkavuna ubaya,

         mmekula tunda la udanganyifu.

     Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe

         na wingi wa mashujaa wenu,

     14 mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako,

         ili kwamba ngome zako zote zitaharibiwa:

     kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita,

         wakati mama pamoja na watoto wao

         walipotupwa kwa nguvu ardhini.

     15 Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli,

         kwa sababu uovu wako ni mkuu.

     Siku ile itakapopambazuka,

         mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.


10:5 [1] Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka.
10:8 [2] Yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni, jina lingine la Betheli kwa dhihaka.

Chapter 11

Upendo Wa Mungu Kwa Israeli

     1 “Wakati Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda,

         nilimwita mwanangu kutoka Misri.

     2 Lakini kadiri nilivyomwita Israeli,

         ndivyo walivyokwenda mbali nami.

     Walitoa dhabihu kwa Mabaali

         na kufukiza uvumba kwa vinyago.

     3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea,

         nikiwashika mikono;

     lakini hawakutambua

         kuwa ni mimi niliyewaponya.

     4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu,

         kwa vifungo vya upendo;

     niliondoa nira shingoni mwao

         nami nikainama kuwalisha.

 

     5 “Je, hawatarudi Misri,

         nayo Ashuru haitawatawala

         kwa sababu wamekataa kutubu?

     6 Panga zitametameta katika miji yao,

         zitaharibu makomeo ya malango yao

         na kukomesha mipango yao.

     7 Watu wangu wamedhamiria kuniacha.

         Hata kama wakimwita Yeye Aliye Juu Sana,

         kwa vyovyote hatawainua.

 

     8 “Efraimu, ninawezaje kukuacha?

         Ee Israeli, ninawezaje kukutoa?

     Nitawezaje kukutendea kama Adma?

         Nitawezaje kukufanya kama Seboimu?

     Moyo wangu umegeuka ndani yangu,

         huruma zangu zote zimeamshwa.

     9 Sitatimiza hasira yangu kali,

         wala sitageuka na kumharibu Efraimu.

     Kwa kuwa mimi ndimi Mungu,

         wala si mwanadamu,

     Aliye Mtakatifu miongoni mwenu.

         Sitakuja kwa ghadhabu.

     10 Watamfuata Bwana ;

         atanguruma kama simba.

     Wakati angurumapo,

         watoto wake watakuja wakitetemeka

         kutoka magharibi.

     11 Watakuja wakitetemeka

         kama ndege wakitoka Misri,

         kama hua wakitoka Ashuru.

     Nitawakalisha katika nyumba zao,”

         asema Bwana .

Dhambi Ya Israeli

     12 Efraimu amenizunguka kwa uongo,

         nyumba ya Israeli kwa udanganyifu.

     Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu,

         hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.

Chapter 12

     1 Efraimu anajilisha upepo;

         hufukuzia upepo wa mashariki kutwa nzima

         na kuzidisha uongo na jeuri.

     Anafanya mkataba na Ashuru

         na kutuma mafuta ya zeituni Misri.

     2 Bwana analo shtaka dhidi ya Yuda,

         atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake

         na kumlipa kwa kadiri ya matendo yake.

     3 Yakobo akiwa tumboni alishika kisigino cha kaka yake;

         kama mwanadamu, alishindana na Mungu.

     4 Alishindana na malaika na kumshinda;

         alilia na kuomba upendeleo wake.

     Alimkuta huko Betheli

         na kuzungumza naye huko:

     5 Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote,

         Bwana ndilo jina lake!

     6 Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako;

         dumisha upendo na haki,

         nawe umngojee Mungu wako siku zote.

 

     7 Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu;

         hupenda kupunja.

     8 Efraimu hujisifu akisema,

         “Mimi ni tajiri sana; nimetajirika.

     Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu

         uovu wowote au dhambi.”

 

     9 “Mimi ndimi Bwana Mungu wenu

         niliyewaleta kutoka Misri;

     nitawafanya mkae tena kwenye mahema,

         kama vile katika siku

         za sikukuu zenu zilizoamriwa.

     10 Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi

         na kusema mifano kupitia wao.”

 

     11 Je, Gileadi si mwovu?

         Watu wake hawafai kitu!

     Je, hawatoi dhabihu za mafahali huko Gilgali?

         Madhabahu zao zitakuwa

         kama malundo ya mawe

         katika shamba lililolimwa.

     12 Yakobo alikimbilia katika nchi ya Aramu;

         Israeli alitumika ili apate mke,

         ili aweze kulipa kwa ajili yake alichunga kondoo.

     13 Bwana alimtumia nabii

         kumpandisha Israeli kutoka Misri,

         kwa njia ya nabii alimtunza.

     14 Lakini Efraimu amemchochea sana hasira;

         Bwana wake ataleta juu yake

     hatia yake ya kumwaga damu naye atamlipiza

         kwa ajili ya dharau yake.

Chapter 13

Hasira Ya

Bwana Dhidi Ya Israeli

     1 Wakati Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka,

         alikuwa ametukuzwa katika Israeli.

     Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali

         naye akafa.

     2 Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi;

         wanajitengenezea sanamu

         kutokana na fedha yao,

     vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari,

         vyote kazi ya fundi stadi.

     Inasemekana kuhusu hawa watu,

         “Hutoa dhabihu za binadamu

         na kubusu sanamu za ndama.”

     3 Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi,

         kama umande wa alfajiri utowekao,

     kama makapi yapeperushwayo

         kutoka sakafu ya kupuria nafaka,

         kama moshi utorokao kupitia dirishani.

 

     4 “Bali mimi ndimi Bwana Mungu wenu,

         niliyewaleta ninyi toka Misri.

     Msimkubali Mungu mwingine ila mimi,

         hakuna Mwokozi isipokuwa mimi.

     5 Niliwatunza huko jangwani,

         katika nchi yenye joto liunguzalo.

     6 Nilipowalisha, walishiba,

         waliposhiba, wakajivuna,

         kisha wakanisahau mimi.

     7 Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba,

         kama chui nitawavizia kando ya njia.

     8 Kama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake,

         nitawashambulia na kurarua vifua vyenu.

     Kama simba nitawala;

         mnyama pori atawararua vipande vipande.

 

     9 “Ee Israeli, umeangamizwa,

         kwa sababu wewe u kinyume nami,

         kinyume na msaidizi wako.

     10 Yuko wapi mfalme wako,

         ili apate kukuokoa?

     Wako wapi watawala wako katika miji yako yote

         ambao ulisema kuwahusu,

         ‘Nipe mfalme na wakuu’?

     11 Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme

         na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.

     12 Kosa la Efraimu limehifadhiwa,

         dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu.

     13 Utungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia,

         lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima;

     wakati utakapowadia hatatoka

         katika tumbo la mama yake.

 

     14 “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi,

         nitawakomboa kutoka mautini.

     Yako wapi, ee mauti, mateso yako?

     Uko wapi, ee kuzimu, uharibifu wako?

 

     “Sitakuwa na huruma,

         15 hata ingawa Efraimu atastawi

         miongoni mwa ndugu zake.

     Upepo wa mashariki kutoka kwa Bwana utakuja,

         ukivuma kutoka jangwani,

     chemchemi yake haitatoa maji

         na kisima chake kitakauka.

     Ghala lake litatekwa

         hazina zake zote.

     16 Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao,

         kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao.

     Wataanguka kwa upanga;

         watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini,

         wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”

Chapter 14

Toba Iletayo Baraka

     1 Rudi, ee Israeli, kwa Bwana Mungu wako.

         Dhambi zako zimekuwa

         ndilo anguko lako!

     2 Chukueni maneno pamoja nanyi,

         mkamrudie Bwana .

     Mwambieni:

         “Samehe dhambi zetu zote

     na utupokee kwa neema,

         ili tuweze kutoa matunda yetu

         kama sadaka za mafahali.

     3 Ashuru hawezi kutuokoa,

         hatutapanda farasi wa vita.

     Kamwe hatutasema tena ‘Miungu yetu’

         kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,

         kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”

 

     4 “Nitaponya ukaidi wao

         na kuwapenda kwa hiari yangu,

         kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.

     5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli;

         atachanua kama yungiyungi.

     Kama mwerezi wa Lebanoni

         atashusha mizizi yake chini;

     6 matawi yake yatatanda.

     Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,

         harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.

     7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake.

         Atastawi kama nafaka.

     Atachanua kama mzabibu,

         nao umaarufu wake utakuwa

         kama divai itokayo Lebanoni.

     8 Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu?

         Nitamjibu na kumtunza.

     Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;

         kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”

 

     9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.

         Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.

     Njia za Bwana ni adili;

         wenye haki huenda katika njia hizo,

         lakini waasi watajikwaa ndani yake.